Mpenzi wangu,
Nikupendaye kwa dhati kutoka moyoni mwangu,
Nakusalimia salamu ya huba iliyoambatana na busu motomoto.
Mpenzi wangu nianze kwa kukushukuru sana kwa barua yako iliyojaa huba ambayo nimeipokea jana mchana nikiwa kazini. Niseme tu nimefurahi sana mpenzi wangu kupata barua yako. Siku zote barua zako huwa tiba mahabuba moyoni mwangu. Kila niusomapo mwandiko wako wa kimahaba huwa napata liwazo la haja moyoni mwangu. Maneno ya kwenye barua yako ni dawa isiyo na kifani ndani ya moyo wangu. Kila mara najikuta moyo wangu unaongeza maradufu upendo juu yako.
Mpenzi wangu, usishangae kuwa nimepata barua jana lakini nimechelewa kukujibu hadi leo ndiyo nimeshika kalamu na karatasi ili nikuandikie ewe malaika wa moyo wangu. Nilipoipata barua yako nilitafakari kwa muda mrefu mno hadi kujikuta nikitokwa na machozi. Hayakuwa machozi ya furaha kama yale yanidondokayo kila wakati nisomapo maneno matamu kutoka kwako ewe mwandani wangu. Maneno ya kwenye barua yako yamenichoma moyoni mwangu mithili ya mkuki wenye ncha kali tena iliyoiva vilivyo kwenye tanuru la moto. Mpenzi wangu, niliyekuchagua mimi mwenyewe kutokana na hisia kali na mapenzi mazito sana niliyonayo moyoni mwangu juu yako, amini bado nakupenda sana.
Mpenzi wangu, nikakiri kwa yakini kuwa nilikuahidi toka miaka mingi sana kuwa pindi nitakapojaaliwa kupata kazi nitakuoa. Nayakumbuka maneno ya ahadi niliyokuwa nikikupa kila mara tulipokuwa tukipata kaupenyo ka kuwa pamoja. Ahadi yangu bado ipo pale pale mpenzi wangu. Moyo wangu, kwa dhati kabisa, bado una dhamira ya dhati ya kukuoa mpenzi wangu nikupendaye kuliko chochote humu duniani, kuliko hata niipendavyo nafsi yangu. Bila wewe mpenzi wangu, dunia hii ina faida gani kwangu?
Mpenzi, nimetokwa machozi kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe. Kwenye barua yako umeandika jinsi unavyokata tamaa kwani sasa ni mwaka moja toka nianze kazi lakini sijatimiza ahadi yangu ya kukuoa. Mpenzi unaona kama nakupotezea muda na unaniomba kama sina haja nawe nikupe nafasi uolewe na mtu mwingine ambaye hata leo hii yupo tayari kuleta posa kwa wazazi wako. Sijui niyaelezeaje maumivu makali ninayoyasikia ndani ya moyo wangu.
Mpenzi wangu, niseme tu ukweli. Ninakupenda mno kuliko hata maana ya neno lenyewe upendo. Ninatamani sana hata sekunde hii hii niwe nimeoana nawe. Lakini, kama nikwambiavyo siku zote, ugumu wa maisha hapa Dar es Salaam hususani kwangu mie mfanyakazi wa kima cha chini ndiyo unaonifanya nikose uthubutu wa kukuoa ewe mpenzi wangu niliyekupa moyo wangu wote, haraka iwezekanavyo kama ambavyo nimekuwa nikikuahidi mara nyingi sana. Mpenzi wangu, moyoni mwangu inaniuma sana maana maisha magumu ninayoyaishi hapa Dar es Salaam kwa kweli yanatishia kwa kiasi kikubwa sana ustawi na uhai wa penzi letu.
Mpenzi wangu, nikwambie nini ili ufahamu kwa kiasi gani akili na moyo wangu vyatamani kwa dhati kabisa kuishi nawe milele yote kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujaalia siku za kuishi humu duniani. Nikwambieje ili ufahamu ni namna gani nalitamani pendo hili lidumu humu duniani na baada ya hapo?
Mpenzi, maisha yangu mfanyakazi wa kima cha chini ni magumu mno. Fikiria mpenzi wangu, kamshahara kangu ambako ni kadogo mno, kanapaswa kalipe kodi ya nyumba, umeme, maji, matibabu, gharama za usafiri na mengineyo chungumbovu. Mpenzi wangu huwezi amini kuna wakati huwa nalazimika kutembea kwa miguu kutoka kazini pale Stesheni mjini hadi nilikopanga Mbagala Kizuiani. Huwa inanigharimu masaa karibia mawili nachapa tu mwendo tena wakati mwingine mvua ikininyeeshea mwili mzima. Sijakwambia tu mpenzi wangu, mara zingine huwa nalazimika kushindia mlo mmoja ama pengine nisile kabisa. We acha tu mpenzi wangu.
Mpenzi, natamani ningekuwa na uwezo wa kukufungulia moyo wangu uyaone yaliyo ndani. Natamani mno tena kupita maelezo kuoana nawe. Kinachonikwamisha mpenzi wangu ni ugumu tu wa maisha ninaokabiliana nao hapa mjini. Sikusudii kukuoa ili uteseke. Sikusudii kukuoa ili nikushindishe njaa. Siyakusudii hayo.
Mpenzi wangu, sikusudii kuuweka uhusiano wetu rehani. Mpenzi sina namna niwezayo kuibadili hali halisi kwa sasa zaidi ya kulazimika kufanya kazi kwa bidii ili pengine bosi wangu anione anipandishe cheo ama kunipa nafasi ya kwenda kujiendeleza kielimu. Lakini tatizo kazini kwetu kumejaa majungu mno kiasi kwamba uchapakazi wangu unanifanya nionekane kimbelembele. Kila mtu ananiona nina kiherehere hadi nalazimika kuwa mpole na goigoi kama wafanyakazi wengine. Kwa mtindo huu sijui ni lini nitafanikiwa kimaisha.
Mpenzi, kweli kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu, sitamani wala siombi uniache na kuolewa na mwingine kwa sababu tu ya hali yangu duni. Machozi yananitoka mno kuyaandika maneno haya. Ninakuomba mpenzi wangu univumilie walau kwa mwaka moja mwingine pengine serikali itatufikiria na kuamua kuboresha hali zetu. Chonde chonde mpenzi wangu.
Mpenzi wangu, najaribu kukwepa kuufikiria mtihani mkubwa unaokukabili kwa sasa. Mapenzi ya kweli ama maisha bora. Najaribu tu kupambana na wivu moyoni mwangu. Najaribu kutamani kuvivaa viatu vyako na kuchagua mapenzi ya kweli. Lakini sipungukiwi imani.
Mpenzi wangu, najua nimekuchosha kwa barua ndefu sana ambayo hata hivyo imeshindwa kujibu swali lako la nitakuoa lini. Ninatumai maelezo yangu pamoja na kutojibu moja kwa moja swali lako, angalau yametoa mwelekeo wa jibu.
Mpenzi wangu, natamani kusema mengi sana zaidi ya haya. Najua hata siku moja dau tupu haliendi joshi na maneno matupu hayajengi nyumba. Ninaloweza kukwambia ni kuwa ninakupenda mno, daima ninakuwaza wewe kwa kuwa umetamalaki moyoni mwangu. Wewe ndilo pambo la moyo wangu. Kwa huba na mahaba yajazayo vibaba na vibaba, penzi langu kwako limeshiba.
Post a Comment